Religion & Spirituality
Unaweza ukawa unafurahia biashara uliyonayo na kufikiri kwamba umefika lakini Mungu ana kitu kikubwa kuliko unachofikiri. Ila hujajua kwamba huko ndani yako kuna kitu gani kimekaa na kwanini ndani yako unaona ndoto kubwa au unaona hujaridhika mahali ulipo kumbe Mungu anajaribu kukusukuma kukuonyesha kwamba ndani yako amekuwekea kitu kikubwa kuliko unacho fikiri. Hivyo usitosheke na mahali ulipo kisukume na usonge mbele na ukimwendea Mungu atakuonesha mahali unapotakiwa kuwa. Mungu alimpa Yusufu miaka 14 ya kutumia zile akili. Na ndiyo maana si suala la kuishi maisha marefu ni suala la kuishi katika mapenzi ya Mungu. Kuna wengine wanaishi maisha marefu na maisha yao hutaki hata kuyasikia, maana ni hasara tu mpaka kwa udongo. Lakini kuna wengine wana maisha mafupi kama ya Yesu, maana yeye alikufa kabla ya kufikisha miaka 40 na ni miaka 3 ndiyo iliyomleta hapa duniani miaka mingine unaona wakiandika habari zake kwa uchache sana. Miaka yake 3 ilibadilisha kila kitu na kuweka alama ambayo shetani hawezi kufuta. Sijajua Mungu amekupa mtu wa namna gani, au kwamba Mungu amekubebesha akili za namna gani ila ninachojua akina Yusufu wako tena yawezekana ni wewe. Wakati ukifika haijalishi uko jela au umesingiziwa Mungu atakutoa tu huko, ikifika saa ya kwako Mungu atatengeneza njia tu hata kama hakuna njia na kukufikisha mahali kila mtu atakutazama na kusema kama si Mungu aliyekuwa pamoja naye huyu mtu na aseme sasa. Na ndiyo maana Yusufu pamoja na kulia alipowaona ndugu zake hakuwa na sababu ya kuwachukia na kuwakasirikia alijua ya kwamba kama si Mungu wasinge fika pale na yeye asingefika pale. Kwa hiyo ukiona watu wanakuchukia na kukupiga vita njiani wakati unasonga mbele huhitaji kuwakasirikia wewe songa mbele maana hao hao wanaokuchukia leo kesho watakuja kukuomba mkate. Kwa hiyo ukiwa na akili kubwa usishindane na vidogo. Usiwe na muda wa kupoteza kwenye vitu ambavyo vinakuletea hasara tu. Nilikuambia akili sio ubongo akili iko ndani ya nafsi na ubongo uko ndani ya mwili lakini Mungu aliviumba vifanye kazi kwa pamoja kwa kushirikiana.