Namna ya kujiandaa kukikabili kipindi hiki cha siku za mwisho (Sehemu ya tatu)

Share:

Listens: 0

Ni Salama

Religion & Spirituality


Tutakusanyika mbele za Bwana tutaimba na kushangilia. Kama Yesu asingekufa msalabani safari yake ingekuwa bure. Maana angeishia kuponya watu na ingekuwa bure tu. Kama asingekufa na akafufuka ingekuwa shida sana. Biblia inasema ulitokea ubishi juu ya kiama ya wafu ule ubishi ulileta mtengano katika dini ya wayahudi na ukatengeneza dini ya masadukayo. Ugomvi wao ulikuwa ni imani yao juu ya kiama ya wafu. Huo ubishi ukaletea mgawanyo mpaka ndani ya kanisa wakati ambao watu wameanza kuokoka. Ilibidi Roho Mtakatifu amsemeshe Paulo aandike barua kwa Wakorintho ili wajue kuwa kama Kristo hakufufuka imani yetu ni bure maana yake haina faida. Kama Kristo hakufufuka tumekuwa masikini kuliko watu wote ambao tunamtegemea Bwana. Kama Kristo amefufuka tunajua na sisi kwamba atatufufua. Kwa sababu hiyo anasema ni tumaini lenye baraka kama ambavyo Tito alivyoandika. Endelea kuimba wimbo huo “Wateule wote tutakusanyika” Wimbo huu ukuandae kufanya sala ya toba. Kama uliokoka ukarudi nyuma rudi tena kwa Mungu. Pia kama unajua kabisa Yesu akija leo huna uhakika kama utaenda nae rudi kwa Bwana. Siku moja nilikuwa kwenye ndege mimi na Rubani mmoja. Tulikuwa wawili tu. Akaniambia akipata shida je ntafanyeje. Basi akaanza kunionesha namna ya kushika usukani wa ndege na namna ya kuendesha ndege. Akanionesha mpaka namna ya kutumia breki za ndege. Sasa nikatazama chini, niliona kulivyo mbali sana. Pia nikaona namna tunavyopita mawinguni. Ghafla nikakumbuka “mstari kuwa tutakusanyika kumlaki Bwana Mungu mawinguni”. Yule Rubani alikuwa kaokoka Nikamwambia kuwa ikipigwa tarumbeta ya kuondoka na Yesu akija hapa kutunyakua tutaenda naye na hii ndege itajijua itakakoenda. Lakini kama Mungu anataka tubaki tutabaki. Ni hatari sana kukaa dakika moja mahali na hujui kama Yesu akitokea hapa utaenda naye. Ni hatari sana kwa sababu Yesu yupo, hata kama huamini kama Yupo. Wainjilisti huwa wanatuambia kuwa kama utaamini Yesu yupo hutakuwa na hasara kama usipomkuta ila utakuwa na hasara sana kama utaamini hayupo halafu ukamkuta. Shida ya wengi wanataka waishi mpaka watakapokuwa wazee ile saa wanakaribia kufa ndipo wanatafuta mchungaji waokoke. Kijana wetu Joshua alikufa akiwa mdogo na wenzake wakaniuliza swali “Baba kwanini Mungu alimchukua Joshua akiwa bado mdogo sana wakati biblia inasema kuwa tunaweza kuishi miaka 70 na tukiwa na nguvu miaka 80. Sasa kwa nini Yeye amekufa mapema sana”. Nikawaambia ni kwa sababu mnasoma mstari mmoja tu. Biblia inasema nitakushibisha kwa wingi wa siku. Unaweza ukaishi miaka zaidi ya 80 au ukaishi chini ya hiyo miaka. Anayesema nimeshiba sio yule mgawaji wa chakula bali ni yule anayekula. Nikawaambia kitu kingine kuwa maisha ya mtu ni kitabu kila siku ni ukurasa. Ndio maana biblia inasema Mungu anatangaza mwisho tangu mwanzo. Kwa hiyo ukiona umezaliwa basi ujue kuwa Mungu alifika mwisho ndipo akaruhusu ukazaliwa na ukaanza kitabu chako cha maisha. Kuna maisha ambayo ni sura maana unaona kabisa hapa kuna ukurasa umeisha hapa ila unajua si ukurasa tu bali ni awamu ya maisha imeisha. Kila mwanadamu anayo hiyo. Mungu amendika siku zetu na ndiyo maana mtunga zaburi anasema Mungu naomba nisaidie kuzijua siku zangu. Kuna vitabu vingine vina kurasa chache sana na ni vitabu vitamu sana. Mwandishi hakuwa na sababu ya kuandika kitabu kikubwa wakati alichokuwa anatakiwa kuandika kimeisha. Kuna vitabu vingine vina kurasa nyingi sana na ukisoma ukurasa wa kwanza na wa pili unakifunga kwa sababu hakina ladha kwa sababu kama ukiandika tu kwa ajili ya kujaza kurasa hata wewe mwenyewe hutarudia kukisoma. Hivyo hivyo hata Mungu pia haandiki tu maisha ya mtu kwa ajili ya kujaza siku. Nikawaambia wale rafiki zake Joshua kuwa kitabu chake kilikuwa ni kifupi sana lakini ni kitamu. Maana kuna vitabu vingine vikiisha unatazama kama kuna mwendelezo wake maana ni kitamu sana. Hicho kitabu hukiachi mahali bali utakiweka mfukoni. Kila baada ya muda utakuwa unakisoma. Yesu hakumaliza miaka 40, na kitabu chake ni kitamu sana mpaka leo tunasoma na hatuchoki kusoma. Hakuna kitu kibaya kama nikikuuliza sasa hivi kuwa ukifa sasa utaenda wapi?. Kama huna jibu lililonyooka ujue unamhitaji Yesu. Maana hutaweza kwenda mbinguni kwa sababu ya mahali unaposali. Hakuna dini iliyokufa kwa ajili ya mtu. Na usije ukajivunia matendo mema maana wakovu ni kipawa hakiji kwa njia ya matendo mema bali ni kwa njia ya imani. Kama unajiona una matendo mema kasimame mbele za Mungu aliye Hai na ndipo utajua kama uko salama!. Kumbuka Isaya alihuburi sura ya kwa hadi sura ya tano. Sura ya sita baada ya kufa kwa mfalme Uzia ndipo alisema mimi ni “mwenye dhambi na midomo michafu”. Sura zote tano hakuona bali sura ya sita ndipo anaona ana mapungufu kwa sababu Mungu alijifunua kwake. Miaka kadhaa tukiwa Tanga kwenye semina nilikuwa nafundisha habari za Jina la Yesu. Ilikuwa ni semina ya siku tano tulikuwa ndani ya jengo. Jengo lile lilikuwa la wenzetu wa imani ya kihindi wanaobudu ng’ombe wakatupa jengo lao tukafanyia semina. Siku ya pili niliitwa Dar es Salaam kwenye masuala ya uchumi. Wazo la kwanza lilonijia ni kutokwenda Mungu akaniambia nenda kwa sababu ile kazi nayo pia nimekupa unatakiwa uende. Nikamuuliza sasa semina ya kesho? akasema upako wa kesho uko juu ya mke wako. Hata kama ningebaki upako ulikuwa juu ya mke wangu maana ndiye aliyekuwa anatakiwa kufundisha. Basi nilienda Dar es Salaam maana kikao kilikuwa saa nane hadi saa kumi, nilipomaliza nikarudi Tanga. Nilipofika ilikuwa majira ya saa tano usiku nikakuta mji umetahatuki, nguvu za Mungu zimeshuka pale watu wamejazwa Roho Mtakatifu sana. Kuna mtoto mmoja alinena kwa siku tatu. Watu walikuwa hawafiki nyumbani wanalala njiani wananena kwa lugha hata wanashindwa kuongea. Ile hali ilitutia hofu sana maana tuliona madhaifu tuliyo nayo na vitu ambavyo Mungu anafanya havifanani kabisa. Mungu alifanya vitu vikubwa sana. Tulienda kumuuliza Mungu na alitujibu mwezi wa kumi tukiwa Kilombero kuwa uchafu unaonekana mahali ambapo kuna nuru. Neno la Mungu na Roho Mtakatifu ni nuru. Mahali ambapo kuna uchafu baada ya kumulikwa na nuru ndipo utaanza kupafanyia usafi. Paulo kadri alivyokuwa anaenda mbele za Bwana aliona udhaifu aliokuwa nao.