Religion & Spirituality
Na Biblia inasema Yesu siku za mwisho hatakuja hapa duniani, kwa sababu maandiko yanasema kile kiti cha enzi kikubwa cheupe, kiti cha hukumu dunia itakimbia na mbingu zitakimbia na kwa sababu hiyo hicho kiti hakitakuwa duniani kwa sababu dunia itakimbia na mbingu zitakimbia. Biblia inasema nikawaona wafu wakubwa kwa wadogo wamesimama katika kiti cha enzi halafu atasimama pale kama hakimu. Sasa hivi ni mwokozi wako lakini ukikutana naye ng’ambo ya pili kama hujaokoka utakutana naye kama hakimu na maandiko yanasema atabagua na kuita majina. Biblia inasema mauti itaitwa iwatoe wafu, bahari na kuzimu itaitwa. Unajua saa nyingine tunafanya kazi ya Mungu tunasahau kuwaambia na kuwahimiza watu juu ya ukaribu wa kurudi kwa Yesu. Tangu watoto wetu wakiwa wadogo kati ya kitu ambacho tumekuwa tukiwasemesha mara kwa mara ni hiki. **Kwenye mambo ya rohoni waishi kama watakufa sasa hivi, na kwenye mambo ya mwilini waishi kama vile hawatakufa maana yake kwenye mambo ya rohoni waishi wakiwa tayari Yesu akishuka sasa hivi wawe tayari, hawana shida ya kutahayari wanaenda pamoja na Bwana, lakini waendelee kupanga maisha yao na kufanya shuguli zao na kupanga mambo mbalimbali kama vile kufa hakupo. ** Na watu wengi wanapanga mambo yao kama vile Yesu hatatokea wakati wowote ule. Na kitu mojawapo katika utumishi ukishapoteza sura ya kurudi kwa Yesu uwe na uhakika utapoteza na uchaji na utapoteza umuhimu wa nyakati, utataka kufanya vitu vyako saa yeyote unayotaka lakini huwezi kufanya kazi ya Mungu saa yeyote unayotaka, huwezi kutii kitu cha Mungu saa yeyote unayotaka. Mungu ameachia kila kitu kwa saa yake na mipango yake na anategemea watu wake sio tu watii Neno lake lakini watii Neno lake katika nyakati na muda aliowawekea kwa sababu nyakati na muda aliowawekea ndizo zinazoweka thamani ya Neno. Jaribu kuzungumza na mtu ambaye hajaokoka kabla hajafa halafu ukasema nina shughuli nyingi halafu kesho ukamkuta amekufa, thamani ya Neno lako la wokovu kwa yule mtu imepotea, lilikuwa na thamani jana alipokuwa hai. Thamani ya Neno liko kwenye muda, ndio anasema wape watu chakula kwa wakati. Shetani akitaka kuvuruga utumishi wako anakamata akili na kwenye akili anashika eneo linaloshughulika na nyakati kwa sababu akilishika hilo huna namna ya kupangua marafiki ambao sio wazuri. Biblia inasema huyu mtu ameshirikiana na watu ambao kwa jinsi ya kawaida asingeshirikiana nao kwa sababu ameona bwana wake amekawia. Maana yake ndani ya nafsi yake akili ziliposhikwa akapoteza kujua ya kwamba Yesu anaweza kutokea wakati wowote ule kwa hiyo akajikuta yuko na marafiki wa aina yeyote ile. Haiwezekani umsubiri Yesu mawinguni SAA yeyote, halafu ukae na mtu yeyote tu, kazi mojawapo ya akili ni kukuchagulia watu. Akili zikibanwa mtu yeyote tu ambaye anaweza kuwa karibu na wewe, anawaza kama wewe hutajua hata namna ya kujikung’uta naye, lakini ukijua ya kwamba Yesu anarudi, mwili unaweza ukapiga kelele unajua umechoka sana! Ni sawa umechoka lakini unaenda mbele za Bwana unakuta Roho Mtakatifu akikuhimiza siku za kurudi Bwana zimekaribia. Wengine wanamfahamu mzee moja aliitwa Aaron Mabondo wa kanisa la Pentecost kule Dar es salaam, ameshafariki sasa alitusaidia sana kwenye kukua ndani ya Bwana, siku alipokaribia kufariki tulienda kuongea naye, mwili wake ulikuwa umechoka, tulikuwa na mke wangu na mke wake alikuwa pale halafu akanitazama usoni akamtazama na mke wangu halafu akasema “wanangu mnisikie mnaniona jinsi nilivyo fanyeni kazi ya Bwana maadam mwili unawaruhusu kusonga mbele, songa mbele kwa sababu mtafika saa hamtaweza kutumika tena” hakumaliza mwezi akafa. Ukiwa na wazo la Yesu kurudi ukisikia basi limeanguka na kuua watu kumi wazo la kwanza ndani yako ni je wamekufa wanamjua Yesu?! Sio swala la huzuni ni swala la kwamba amekufaje! Ukiona ndani hilo swali halipo unahitaji kurudi kwa Bwana ujue akili zako zimebanwa. Kwa sababu shetani atakuchanganya kama sio kurudi kwa Yesu atakuchanganya kuchukua mafundisho ambayo sio sahihi. Atahakikisha anaondoa kitu cha kurudi kwa Yesu kisiwe sehemu ya maisha yako na wakati kinatakiwa kuwa sehemu ya maisha yako. Maana yake kaa mkao ili Yesu akikuitia mahali popote unaenda. Kitu mojawapo kilichomponza yule mtumishi akapelekwa mahali ambapo kuna kilio na kusaga meno ni kwamba alisema Bwana wake amachelewa kurudi. Akili zake zilimwingizia kitu cha tofauti, shetani alibadilisha mistari ile ambayo Mungu aliyompa Adamu maelekezo na alienda kwenye fikra, akaanza kuweka kiulizo kwenye ahadi ya Mungu na Neno la Mungu. Na huyu mtumishi Bwana wake amemwambia mimi karibu narudi niandalie watu wangu niandalie kanisa langu halafu yeye anasema bwana amekawia kurudi! Hilo wazo amelipata wapi? Lazima shetani ametumbukiza kitu kwenye fikra zake, anaanza kusema Yesu haji, mbona mwaka juzi, mwaka jana tumeendelea hivo hivo. Wewe unatazama vitu kwa jinsi ya mwili unasahau kwamba lazima utazame sehemu zote mbili kwa sababu kurudi kwa Bwana kunategemea, wengine siku atakapotokea atawakuta wakiwa hai na watabadilishwa miili yao kufumba na kufumbua watanyakuliwa, lakini kuna wengine wanatakiwa walale katika Bwana siyo katika dini, bali kuhakikisha kwamba una Yesu ndani yako. Ushuhuda Nilikuwa naongea na rafiki yangu moja niliyekuwa nafanya naye kazi ofisi moja mahali, halafu akaugua nikamfuata nyumbani kwake hajiwezi kabisa hata kusimama kwenye kitanda, nikamwambia “ndugu najua wewe ni Mkristo mzuri na tunasali wote lakini najua hujaokoka na mimi nataka nikuongoze sala ya toba umpokee Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Huu ni mtaji, ni mtaji wa kuishi milele na pia ni mtaji wa kuishi na Yesu duniani, na akikuita saa hii ni mtaji wa kwenda mbinguni, je unasemaje?” akasema “Niko tayari”. Nikamwongoza sala ya toba kitandani na baada ya mwezi mmoja akafa.