Kumwamini Mungu kwa kumfuata Yesu Kristo (Sehemu ya Pili)

Share:

Listens: 0

Ni Salama

Religion & Spirituality


KUMWAMINI MUNGU KWA KUMFUATA/KUPITIA KWA YESU KRISTO. Ukisoma Luka 8:12 “Wale wa karibu na njia ndio wasikiao, kisha huja Ibilisi akaliondoa hilo neno mioyoni mwao, wasije wakaamini na kuokoka.” Pia Warumi 1:28 “Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.” Ufahamu ulioko ndani ya akili zisizofaa zilifanya wamkatae Mungu. Kwa hiyo akili itafanya mtu amkubali au amkatae Mungu. 2 Wakorintho 11:3 “Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.” Shetani akitaka uache usafi na unyoofu wa Kristo, hashambulii roho yako kwanza; anashambulia fikira zako kwanza au kinachokusaidia kufikiri, yaani akili. Shetani alipotaka kufikia roho ya Adamu na Hawa alishambulia fikra zao, kwa hiyo akitaka kuzuia watu wasimwamini Yesu kama jinsi Mungu alivyomtuma, atashikilia fikira. Ukisoma 2 Wakorintho 4:3‭-‬4 “Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.” Mathayo 22:36‭-‬37 “Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.” Akimaanisha kuwa akili zako ziwe na namna fulani ziweze kushiriana na roho na imani la sivyo kumpenda Mungu wako kutapwaya mahali. 2 Timotheo 3:8‭-‬9 “Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani. Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa dhahiri.” Kinachofanya wapingane na kweli ya Mungu ni akili zao kwa sababu zimeharibika tofauti na kiwango Mungu anachotaka, na kwa sababu hiyo zile akili zinapingana na ile kweli na kusababisha kuwa mbali na imani na kukosa kufanya kazi na kushiriana kama zilivyokusudiwa kushiriana. Unaweza ukawa na msimamo mkali kabisa ukifikiri ni msimamo wa kiroho, kumbe ni akili zako zimekuwekea ugumu usielewe na usisogee. Tuangalie 1 Yohana 5:20 “Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.” Kazi mojawapo ya akili ni kumjua Yeye Aliye wa Kweli. Kwa nini nimeanza na huo mfano? Ni kwa sababu watu wengi sana hawajajua ya kwamba Mungu aliweka hivi vitu viweze kufanya kazi pamoja. Nilishangaa sana nilipokuwa nikisoma Biblia na kufutalia uumbaji wa mwanadamu na zaidi pale Mungu aliposema na tumuumbe mtu kwa mfano wetu na akampa mwili, kwa sababu Mungu hana mwili kama tulio nao ni roho peke yake ambayo inaruhusiwa kuishi kwenye maeneo mawili kwa wakati mmoja bila shida. Mwanadamu aliruhusiwa na aliumbwa aweza kuishi katika ulimwengu wa kimwili na wa kiroho kwa wakati mmoja. Aweze kuishi katika ulimwengu wa kimwili, lakini aweze kuwasiliana na kuishi katika ulimwengu wa kiroho bila shida. Mungu alipokuwa anataka kushirikiana na sisi kutusaidia ilibidi atafute dada mmoja aitwaye Mariam apite kule ndani achukue mwili, na ndiyo maana Biblia inasema mwili nilikuwekea tayari la sivyo ingekuwa ngumu sana kutembea kama sisi na kufa pale msalabani, ilibidi lazima awe na mwili kama wetu. Maana maandiko yanasema kuna miili ya duniani na miili ya mbinguni. Asingeweza kutumia mwili wa mbinguni kuja kutusaidia, ilibidi lazima awe na mwili wa duniani na ndiyo maana Biblia inasema alivua utukufu wake ili aweze kuja duniani. Na Mungu alimuumba mtu kwa namna ambavyo hawezi kuishi katika kiwango ambacho Mungu alikikusudia bila Mungu na ndiyo maana tuliumbwa kwa mfano wake na kila kitu kingine kiliumbwa kwa mfano wa hicho kitu. Lakini mwanadamu peke yake ndiye ambaye alizuiwa asizae kwa mfano wake. Maana hatukuumbwa kwa mfano wa mwanadamu bali kwa mfano wa Mungu, lakini tukaitwa wanadamu ili tusizae mfano wa wanadamu bali tuzae mfano wa Mungu. Mwanadamu alipomkataa Mungu ule uzima wa Mungu na sura ya Mungu ndani viliondoka, maana alimkataa na akakubali roho ya upande mwingine ile roho ya giza kuja kutawala maisha yake.