Religion & Spirituality
Biblia haisemi wanaume tukae na wake zetu kiroho, kwa hiyo usijaribu kukaa na mke wako kiroho, kaa nae kwa akili. Ndani ya akili hizo Mungu atakupa neema ya kumsaidia kumpa heshima anayostahili. Lakini kuona ile nafasi kwa jinsi ya mwili ni chombo kisichokuwa na nguvu lakini katika ulimwengu wa roho wana nguvu kuliko sisi! Kwanini Mungu ameumba jambo jipya mwanamke atamlinda mwanaume wanawake ni walinzi wazuri sana katika ulimwengu wa roho, wana nguvu za kiroho kuliko wanaume lakini inapokuja kwenye maisha ya kawaida Biblia inasema mpe heshima maana ni kiumbe dhaifu. Unaweza ukampenda mke wako lakini usimheshimu, Biblia inasema kama warithi pamoja wa neema,je huwa unamshirikisha mke wako kwa kiwango gani kitu ulichonacho? Kuna watu ambao vitu vyao ni siri kiasi kwamba hata akifa ni shida kujua hata alikuwa na account wapi, alikuwa pesa kiasi gani, viwanja vingapi! Hata mke hajui na siku akifa anaanza kuhangaika kama mtu mwingine. Tito 2:3-5 Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe. Biblia inatuambia wanawake watu wazima wamepita mahali wameona umuhimu wa akili ndio maana biblia inasema wasaidieni hawa wanawake vijana watieni akili.Mwanamke anatumia akili kumpenda mume wake na mwanaume anatumia akili kumpa heshima mke wake. Hapo roho haitajwi katika kupenda wala kumpa mke heshima bali ni akili inatumika. Biblia inasema na kuwapenda watoto wao, maana unaweza ukawapenda watoto yatima lakini wa kwako usiwapende.Haitoshi tu kusema unawapenda watoto maana unaweza ukasahau kuwapenda watoto wako mwenyewe. Ndio maana biblia inasema wanawake wawatie wanawake vijana akili za kuwapenda watoto wao na waume zao, kuwa wenye kiasi, na kuwa safi. Kwa hiyo mwanamke akiwa mchafu shida ni akili zake. Kwa hiyo kama pepo limemfanya kuwa mchafu ina maana limeshika akili zake, maana inatakiwa akili zitumike ili kumfanya kuwa safi. Mwanamke anatakiwa kufanya kazi nyumbani mwake. Maana anaweza fanya kazi kwingine lakini nyumbani mwake asifanye kazi. Pia wanawake wanatakiwa kuwa wema na kuwatii waume zao wenyewe. Kuna baadhi wanawake wanawatii sana wachungaji zao kuliko waume zao, maana si vibaya kumtii mchungaji. Lakini kumbuka mume akimfukuza huyo mke wake, mchungaji hawezi kumuoa. Pia mke wa mchungaji nae akikaa vizuri kwenye nafasi yake endapo akienda mwanamke aliyefukuzwa na mume wake akaenda kwa mchungaji kuomba msaada, atamuuliza “ unaenda wapi kwani huna kwenu?”. Hata akijieleza kuwa kaenda ili kupata ushauri, maana wanaweza mvumilia kwa siku chache hata kama watampa hifadhi ila baada ya muda mfupi watamuuliza kwanini haendi kwao kama kafukuzwa na mume wake? Maana hatakiwi kukaa tena kwa mchungaji wake.