Religion & Spirituality
Mtu aliyekuwa anatakiwa kwenye hii nafasi alitakiwa awe ana akili ya miaka 14 kusaidia Misri na nchi za jirani. Alitakiwa awe ana hekima pamoja na Roho wa Mungu ili kuweza kukamilisha jukumu hilo. Yusufu aligundua kuna kitu Farao alitakiwa akitolee nafasi (position) kwa sababu anaweza patikana mtu mwenye akili lakini asiwe na mahali pa kutumia akili zake. Kuna watu wana akili lakini hawana hekima na wengine wana hekima akili hawana. Yusufu alikuwa na hivyo vyote pia alikuwa na Roho wa Mungu ndani yake. Kwa maana hiyo Mungu alimpa nafasi ili aweze tumia akili, hekima na Roho ya Mungu iliyokuwa ndani yake katika kufanya alichotakiwa kufanya kwa miaka 14. Mwanzoni kabisa Yusufu aliotea ndoto akiwa na miaka 17 lakini alipewa kuwa waziri mkuu akiwa na miaka 30, kwa hiyo miaka 13 ilimtesa kufukia mahali pa kuweza kutumika miaka 14. Kwa sababu alipitia wakati mgumu sana miaka hiyo 13 maana Mungu alimleta duniani kwa kazi hizo kubwa. Moja ya kazi ni kuhakikisha ile miaka 14 pale Misri akili zake zinatumika sawasawa kwa sababu alisema Mwanzo 45:7-8 “Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri.” Maana yake amekuwa na akili iliyomfanya kuwa baba kwa Farao mahali ambapo kwa jinsi ya kawaida isingewezekana pia akawa baba kwa taifa la Misri na kwa ndugu zake. Yusufu ndoto (vision) yake ilikuwa ya contract ya miaka 14. Lakini alifanya vizuri kiasi ambacho hakustaafishwa baada ya muda wake kuisha bali aliendelea na kazi mpaka alipo kufa. Kumbuka Yusufu alipewa akili ya kusaidia ndugu zake lakini ndugu zake walimkataa hata alipoenda kuwapelekea chakula walipomwona walimkasirikia wakaanza kupanga kumu ua. Sasa fikiria walitaka kuua akili ya namna gani kwa kubebeshwa kitu cha aina gani. Kwa hiyo ili wasimuue wakakubaliana kumtumbukiza kwenye kisima kisicho na maji halafu wakafikiria tena kuwa wamuuze kama mtumwa bila kujua thamani ya akili iliyokuwa inauzwa. Waishmaeli nao wakaja kumuuza kwa Potifa na Potifa baadae akamtazama akagundua Yusufu ana baraka fulani na sio akili tu. Potifa akamweka Yusufu kuwa kiongozi wa kila kitu nyumbani kwake. Aliposhindwana na mke wa Potifa akaishia jela, sasa fikiria ni akili gani ambayo ilikuwa imefungwa jela. Kuna wengine wamefungwa jela (jela hizi za kawaida kwa makosa halali au kwa kusingiziwa/kuonewa) na wana akili kama ya Yusufu. Pia mkuu wa jela akagundua baraka zilizokuwa juu ya Yusufu na kumpa cheo. Naye Yusufu akamsaidia mtu mkubwa sana katika taifa la Misri kwa kumtafsiria ndoto yake na akamwambia akirudi kazini kwake amkumbuke ili aweze toka jela. Lakini yule mtu alimsahau kwa hiyo Yusufu alisahauliwa jela miaka miwili. Ninaposoma hizi habari huwa namshangaa sana Mungu. Inawezekana umesahauliwa huna nafasi yoyote, huna kazi lakini hujui akili uliyobeba na inawezekana hata waliokuzunguka hawajui akili uliyobeba.Maana unaweza ukawa na upako lakini kuna watu wanaojaribu kutafuta kukuua na Mungu amenyamaza. Unaweza ukawa ndani ya birika na ndugu zako wakakuchukia kabisa. Usije ukafikiri Mungu amekuacha maana nguvu za Mungu ziko pamoja na wewe. Inawezekana unaishi maisha kama ya kitumwa lakini mkono wa Bwana uko pamoja na wewe. Yusufu alikuwa na Mungu kwenye kila mazingira toka anauzwa, alipopelekwa mahakamani kwa sababu ya mke wa Potifa Mungu alikuwa pamija nae. Alipokuwa jela alikuwa pamoja na Mungu kwa hiyo kila sehemu Mungu alikuwa pamoja nae. Kwa hiyo usije ukafikiri waliofungwa jela hawana Mungu wako pamoja na Bwana. Shetani alikuwa anagombana na akili za Yusufu ili zisipate nafasi ya kutumika maana alikuwa ana akili ya kusaidia familia yake lakini alinyimwa heshima nyumbani kwake. Akili alilozokuwa nazo Yusufu zilikuwa na uwezo wa kumsaidia baba yake lakini aliondolewa nyumbani kwao na kukatiwa mawasailiano na baba yake ili ajue kwamba amekufa. Shetani alikuwa akiwinda baba yake yaani mzee Yakobo asipate msaada wa akili za Yusufu. Unaweza ukawa unafurahia biashara uliyonayo na kufikiri kwamba umefika lakini Mungu ana kitu kikubwa kuliko unachofikiri. Ila hujajua kwamba huko ndani yako kuna kitu gani kimekaa na kwanini ndani yako unaona ndoto kubwa au unaona hujaridhika mahali ulipo kumbe Mungu anajaribu kukusukuma kukuonyesha kwamba ndani yako amekuwekea kitu kikubwa kuliko unacho fikiri. Hivyo usitosheke na mahali ulipo kisukume na usonge mbele na ukimwendea Mungu atakuonesha mahali unapotakiwa kuwa. Mungu alimpa Yusufu miaka 14 ya kutumia zile akili. Na ndiyo maana si suala la kuishi maisha marefu ni suala la kuishi katika mapenzi ya Mungu.